Katika hali ya kuvijengea uwezo na kuviongezea nguvu ya ushindani hasa kimataifa vilabu vya Simba Sc na Young Africa Sc,Bank za NMB na CRDB Mkoa wa Kigoma zimeendesha mafunzo elekezi kwa wanachama wa Vilabu hivyo ya namna ya kujisajili na kuwa mwanachama hai.
Meneja biashara wa CRDB Deus Mwita amesema timu hizi ni mali ya umma hivyo ni muhimu kwa kila mwanachama kuchangia Ada ya uanachama ili kuviwezesha kufanya usajili bora na wenye tija ili viwe na ushiriki mzuri kimataifa.
Kwa upande wa afisa wa benki ya NMB Anastazia Ganja amesema licha ya mchango wa mwanachama kuichangia timu yake,pia atapata bima ya maisha ambapo akifariki au kufiwa atapewa kiasi cha shilingi milioni mbili kwa ajili ya kumsaidia mazishi na shughuli nyingine za msiba.
Mapema mwezi Julai Vilabu vya Simba na Yanga viliingia makubaliano na Benki hizo ili kuwafikia wanachama na mashabiki kiurahisi ambapo kila mwanachama anatakiwa kuchangia Shilingi 24,000/=na Shabiki akitakiwa kuchangia Shilingi 12,000/=kwa kila mwaka.