TANZANIA

Serikali Ya Tanzania Kushirikiana Na Wadau Kutokomeza Ulemavu Wa Kutokuona

JULAI 31, 2023
Border
news image

Serikali ya Tanzania imetoa wito kwa wadau wa maendeleo nchini kushirikiana kwa karibu katika kuboresha huduma za afya ya macho ili kuzuia ulemavu wa kutokuona na upungufu wa kuona kwa jamii za Kitanzania

Wito huo umetolewa leo Jijini Dodoma na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Ahmadi Makuwani katika ufunguzi wa kikao kazi cha kupokea wasilisho la Mradi mpya wa Afya ya Macho unaotekelezwa chini ya ufadhili wa Shirika la Sightsavers.

Aidha Dkt. Makuwani amesema kuwa kupitia ushirikiano wa Serikali pamoja na Wadau wataweza kupunguza changamoto za matatizo ya macho Tanzania ambapo Mfumo wa Afya ya Macho unakabiliwa na changamoto mbalimbali za miundombinu, watumishi, vifaa, vifaa tiba na teknolojia.

Hata hivyo Dkt. Makuwani amesema kuwa Mradi huo unalenga kuboresha Afya ya Macho katika azma ya kuchangia kuzuia ulemavu wa kutokuona unaoepukika unaenda kutekelezwa kwenye mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro

“Tunafahamu kwamba kuna takriban watu milioni 39 Duniani kote wenye ulemavu wa kutokuona na milioni 245 wenye upungufu wa kuona na takriban asilimia 90 ya watu wenye ulemavu wa kutokuona wanaishi katika nchi za kipato cha kati na chini. Hata hivyo, asilimia 80 ya ulemavu wa kutokuona unaweza kuzuiwa na kutibika” amesema.

Ameongeza kwa kusema kuwa, kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani, Tanzania inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 620,000 wenye ulemavu wa kutokuona na watu takriban Milioni 2 wenye upungufu wa kuona.

Dkt. Makuwani amelipongeza shirika la Sightsaver kwa kuendelea kufadhili mradi wa macho na kuwasihi kuendelea kutoa michango ya kuboresha mradi huu wa macho pamoja.

Dkt. Makuwani amewataka wadau kutoa huduma nafuu ya vifaa tiba kwa wananchi wa chini ili waweze kumudu gharama pamoja na kuwafikia wanafunzi walioko mashuleni.

“Nipende kuwasihi washiriki wa kikao hiki kuwa makini katika kusikiliza na kutoa michango itakayokwenda kuboresha mradi huu na kuleta ufanisi mzuri wenye matokeo chanya kwa jamii yetu”, amesisitiza Dkt.Makuwani.

Vile vile amewataka washiriki hao kuzingatia uwepo wa afua zitakazoenda kuongeza usawa kwa jamii itakayohudumiwa, mathalani afua za kuongeza uelewa wa lugha za alama kwa watumishi wa afya na afua za kuwezesha ufikiwaji wa majengo kwa watu wenye ulemavu na wazee (matumizi ya ramps badala ya ngazi).

Aidha, amesema afua zisiwaache watoto shuleni kwani kupitia vipimo na elimu huduma endelevu ya Afya ya macho nchini.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania