TANZANIA

Masoko Ya Madini Tanzania Yaendelea Kupaisha Sekta Ya Madini

JULAI 30, 2023
Border
news image

Wastani wa tani 1.48 za dhahabu zauzwa kwa mwezi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini nchini Tanzania Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa wastani wa mauzo ya madini ya dhahabu katika masoko ya madini kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2022 hadi Juni, 2023 ni tani 1.48 kwa kila mwezi kutokana na usimamizi mzuri wa masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 94 vilivyoanzishwa nchini humo hivyo kupelekea Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo kwenye Kikao cha Tume kilichofanyika jijini Dodoma Tanzania kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Madini kwa kipindi cha miezi mitatu kilichoshirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Makamishna wa Tume ya Madini na menejimenti ya Tume iliyoshirikisha Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo.

Amesema kuwa, kiasi kikubwa cha dhahabu kuuzwa katika masoko kwa mwezi kilikuwa ni tani 1.71 kwa kipindi cha mwezi Oktoba, 2022 na kiasi kidogo zaidi kuuzwa kilikuwa ni tani 1.21 kwa kipindi cha mwezi Februari, 2023.

Ameongeza kuwa katika kipindi husika, kiasi cha dhahabu kilichopatikana kupitia masoko ya madini kilikuwa ni tani 17.70 zenye thamani ya shilingi trilioni 2.129 ambapo mapato ya Serikali yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na mrabaha na ada ya ukaguzi kutokana na mauzo hayo yakiwa ni shilingi bilioni 149.

Ameongeza kuwa, kufuatia ongezeko la uzalishaji baada ya kipindi cha mvua ambacho huwa na athari kubwa kwa wachimbaji wadogo wa madini na usimamizi mzuri, kiwango cha uzalishaji kiliongezeka katika mwezi Machi hadi Juni 2023 sambamba na mauzo ya madini mengine ikiwa ni pamoja na madini ya bati, almasi, tanzanite na aina nyingine za madini ya vito vya thamani.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amesema kuwa ili kupunguza ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, Tume imeendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini nchini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira hali iliyopelekea kupungua kwa ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma akielezea kasi ya utoaji wa leseni za madini amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022-2023, Tume ilitoa jumla ya leseni za madini 9,642 ikiwa ni asilimia 105.10 ya lengo la kutoa leseni 9,174 kwa kipindi husika.

Aidha ameongeza kuwa “ Katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni, 2023 maombi mapya ya leseni za madini 3,837 yaliwasilishwa yakiwa ni pamoja na ya leseni za utafutaji madini, uchimbaji wa kati, uchimbaji mdogo, uchenjuaji wa madini na biashara ya madini ambapo yaliridhiwa kwa ajili ya kupatiwa leseni za madini,” ameongeza Profesa Mruma.

Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo akiwasilisha taarifa ya usimamizi wa utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2023 Tume ilipokea jumla ya mipango iliyowasilishwa kwa mara ya kwanza 143 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ambapo mipango 142 ilipitishwa baada ya kukidhi vigezo.

Ameongeza kuwa, ili kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini, Tume imekuwa ikitoa elimu kwa kampuni zinazomiliki leseni za madini na wadau wa madini sambamba na kufanya majukwaa na warsha mbalimbali kuhusu utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.

Wakati huo huo akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Tume ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini na kuongeza kuwa Serikali na watanzania wote wana matarajio makubwa, hivyo ni vyema bidii ya kazi, ubunifu na uzalendo vikatangulizwa mbele kwa maslahi ya Taifa.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na biashara ya madini, kuimarisha usimamizi kwenye masoko ya madini na vituo vya madini vilivyoanzishwa nchini, na kuongeza kasi ya utoaji wa leseni za madini.

“Aidha, kama Tume ya Madini tunajipanga kuimarisha usimamizi kwenye masuala ya afya na mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ili kupunguza madhara ya kimazingira na afya katika maeneo husika huku tukihakikisha wananchi wanashiriki vyema kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini sambamba na migodi kuboresha huduma za jamii,” amesema Profesa Kikula.

Oliver G Nyeriga