TANZANIA

Wizara Ya Maendeleo Ya Jamii Kuimarisha Uratibu Na Wizara Za Kisekta

FEBRUARI 28, 2024
Border
news image

Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum nchini Tanzania Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameongoza kikao cha Wataalamu wa Kisekta wa Kada ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara hiyo pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa lengo la kuweka mkakati ya pamoja ili kuimarisha ufanisi wa utekelezaji na ufuatiliaji wa shughuli za Maendeleo ya Jamii kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Dkt. Gwajima, amefungua kikao hicho katika Ofisi za Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jijini Dodoma.

“Mimi na Waziri mwenzangu mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa tunatambua Dhamira ya Mhe. Rais ya kuunda Wizara hii kwa ajili ya Jamii ya Watanzania kwamba ni kuhakikisha inachochea Kasi ya maendeleo ya watu, hivyo tumekubaliana kuimarisha umoja, ushirikiano na mshikamano katika ufuatiliaji wa utekelezaji na kwamba, wataalamu waje na mkakati shirikishi katika kuongeza Kasi ya utekelezaji wa majukumu yanayotuhusu".

Amesema Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Wataalamu ni lazima watengeneze utaratibu wa kuunganisha mifumo ili kuwasaidia wananchi ili kuamsha ari ya utekelezaji wa mifumo na mtaalamu mmoja mmoja katika ngazi zote.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe amesema kikao hiki kimekuja wakati muafaka huku akimshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa jitihada zake za kuhakikisha matokea chanya yanapatikana.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Ummy Wayayu ameshukuru hatua hiyo ya kuzikutanisha Wizara hizo mbili na kuahidi ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika kuimarisha mifumo hadi ngazi ya chini.

MTV Tanzania