TANZANIA

Wizara ya Madini Tanzania Kurusha Ndege ya Utafiti Geita

SEPTEMBA 27, 2023
Border
news image

Kutokana Wizara ya Madini nchini Tanzania kutambua mchango wa wachimbaji wadogo wa madini katika pato la Taifa, hivyo ipo na mkakati wa kufanya utafiti wa kina kwa kurusha ndege maeneo mbalimbali ikiwemo Geita ili kupata taarifa sahihi za uwepo wa madini katika maeneo husika.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini nchini Tanzania Mhe. Anthony Mavunde wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita katika kongamano la kuibua fursa za madini pamoja na kujadiliana juu ya changamoto zinazowakabili wachimbaji wado

Mhe.Mavunde aliongeza kuwa Wizara ya Madini ipo katika mkakati wa kuongeza taarifa za utafiti wa kina wa madini kwa lengo la kufungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi .

Akifafanua kuhusu hali ya utafiti nchini Mhe. Mavunde alisema kuwa kwasasa Serikali imefanya utafiti wa kina kwa asilimia 16 ya eneo la nchi ambayo taarifa zake ndizo zinazotumika kuendeleza miradi ya uchimbaji madini.

Vilevile , Mhe.Mavunde aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa taarifa hizo Serikali imepanga ifikapo mwaka 2030 iwe imefanya utafiti wa kina nchi nzima ili kubaini maeneo yote yenye rasilimali madini , hii itasaidia kuongeza wigo kwa wachimbaji wadogo ,wakati na wakubwa tofauti na ilivyo sasa.

Akielezea kuhusu mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa , Mhe. Mavunde alisema sekta ya Madini inaendelea kupaa na mpaka sasa inachangia kiasi cha asilimia 9.1, hii ni kwa taarifa za utafiti wa asilimia 16 tu, hivyo kwa kuongeza taarifa za kina sekta ya Madini itakuwa kinara katika uchangiaji katika sekta ya madini.

Awali , katika Kongamano hilo Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ziliwasilisha mada mbalimbali juu ya mnyororo mzima wa sekta ya Madini ikiwa pamoja na mpango wa kuwainua wachimbaji wadogo ili wafanye uchimbaji wenye tija na uhakika.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa Geita, Mbunge wa Geita Mjini,Taasisi za Fedha , Wakuu wa Taasisi za Umma na viongozi wa Vyama vya Wachimbaji wadogo.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania