TANZANIA

Waziri Mkuu Ethiopia Kufanya Ziara Tanzania - Mhe. Makamba

FEBRUARI 28, 2024
Border
news image

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Dkt. Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 29 Februari hadi 02 Machi, 2024 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Dkt. Abiy atapokelewa rasmi Ikulu, Dar es Salaam tarehe 01 Machi, 2024 na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Lengo la ziara hii mbali na kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, inalenga pia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ethiopia ambazo zimekuwa zikishirikiana katika maeneo ya biashara na uwekezaji, elimu, utamaduni, usafirishaji wa anga, kilimo, mifugo, udhibiti wa uhamiaji holela, ulinzi na usalama.

Tanzania na Ethiopia zina uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wa kihistoria ambao ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia, Hayati Haile Selassie. Viongozi hawa walishirikiana bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika ni miongoni mwa Viongozi Waanzilishi 32 wa Umoja wa Afrika wakati huo OAU mwaka 1963.

Aidha, mbali na ushirikiano wa kidiplomasia, Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta ya anga ambapo mwaka 2016 hadi 2023 jumla ya marubani 75 na wahandisi 25 kutoka Tanzania wamepokea mafunzo katika ngazi tofauti nchini Ethiopia. Hivyo ni wazi kuwa, ziara hii itafungua milango zaidi ya ushirikiano kati ya Shirika la Ndege la Ethiopia na Shirika la Ndege la Tanzania – ATCL katika kujiendesha kibiashara.

MTV Tanzania