TANZANIA

Waziri Masauni Asema Jeshi la Polisi Tanzania Lipo Imara Nakuwaonya Wahalifu Watafute Kazi Nyingine

SEPTEMBA 4, 2023
Border
news image

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ametoa onyo kali kwa wahalifu nchini kuacha mara moja kufanya uhalifu badala yake watafute shughuli nyingine za kiuchumi kwa kuwa Jeshi la Polisi lipo macho katika kuhakikisha ulinzi na usalama unadumishwa ipasavyo.

Waziri Masauni ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kituo cha Polisi Mavurunza, Wilaya ya Kipolisi Kimara, Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, ambacho hadi kukamilika kwake kimegharimu Shilingi million 100 huku wananchi wa Mtaa huo wakichangia shilingi milioni 70.

"Niwahakikishie, hakuna mhalifu atakayevuka katika mipaka ya Jeshi la Polisi, hatushindwi, hivi juzi Mkoani Njombe ‘walitubipu’ shughuli yao imeisha usiku wa leo.. Jeshi la Polisi na Makamanda ni imara na wananchi wanaonesha mshikamano katika kipindi hiki chenye shughuli nyingi za kiuchumi, Dar es Salaam ni tulivu, Tanzania ni salama." Alisema Masauni.

Hata hivyo, Waziri Masauni amelitaka Jeshi hilo kutoa huduma nzuri kwa wananchi na kuhakikisha haki inatolewa sambamba na kushughulikia kero za wananchi kwa haraka na kwa weledi.

“Najua wapo baadhi ya askari nchini wanafanya mambo kinyume na kanuni za Jeshi la Polisi, Jeshi linafuatilia na kuwachyukulia hatua, na pia kwa upande wa Serikali baada ya malalamiko ya wananchi Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Kamati ya Tume ya Haki Jinai kuangalia nini kifanyike ili kuimarisha zaidi Jeshi la Polisi,” Alisema Masauni.

Ameongeza kuwa, kituo hicho kilichojengwa kwa nguvu ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali kupitia Ofisi ya Mbunge hadi kukamilika kwake kitapunguza adha ya wanachi kwa kufuata huduma katika vituo vilivyo mbali na makazi yao vikiwemo vituo vya Polisi Gogoni na Urafiki.

"Hawa wananchi wa Mavurunza hakika ni mfano mzuri wa kuigwa katika kuonesha nia na kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuweka usalama mbele, kitunzeni kituo hiki na jeshi litatoa huduma kwa haki na wakati," Alisema Masauni.

Katika kuimarisha usalama katika ngazi za Kata, Waziri Masauni alisema dhamira ya Serikali ni kuimarisha vyombo vya usalama na ongezeko la bajeti la asilimia 32 pia imeelekezwa katika kupeleka usafiri kwa Polisi Kata na Wilaya, na ameelekeza uendelezwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi na kuwataka vijana kujiunga na vikundi hivyo ili kudumisha ulinzi na usalama katika mitaa wanayoishi.

Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Murilo amewashukuru wananchi wa Mavurunza kwa kutambua masuala ya kiusalama na kushiriki katika ujenzi wa kituo hicho.

“Niwahakikishie kuwa kituo hiki kitatumika kama ilivyokusudiwa kiusalama na kutoa haki, askari watakaotoa huduma kituo hiki wazingatie nidhamu na uadilifu, Sitegemei wananachi kukasirika na kuchoma moto kituo hiki kwa huduma mbovu zitakazotolewa na nitafuatilia hili kwa ukaribu zaidi,” Alisema Murilo na kuongeza;

“Jeshi la Polisi halina huruma na wahalifu na litaendelea kuhakikisha wananachi wanafanya shughuli zao za kiuchumi kwa amani na usalama usiku na mchana ili kukuza uchumi wa Nchi na uwekezaji kama Serikali ya awamu ya sita ilivyodhamiria.”

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba alisema katika kuhakikisha usalama unadumishwa atashirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha jijini hilo linakuwa salama na wananchi wanafanya shughuli zao kwa amani.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, amemshukuru Waziri Masauni kwa kuja kufungua kituo hicho, na pia amewapongeza wananchi wa eneo la Mavurunza katika jimbo lake kwa kujitoa katika ujenzi wa kituo hicho ambacho kilidumu kwa muda wa mrefu.

“Najua Askari wetu hawana chama na hawatatoa huduma kwa upendeleo ila kituo hiki kimejengwa kwa nguvu kubwa na Chama cha Mapinduzi kupitia uongozi wa Kata, Mhe. Waziri tuna ahadi kubwa tano ambazo tuliahidi kwa wananchi wa hapa Kimara ikiwemo ujenzi wa kituo hiki, barabara ya Kikwete Highway ambayo ina urefu wa Kilomita Saba, na inatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2025.

Barabara hiyo itatua Bilioni 17na tayari imeidhinishwa kwa ujenzi pamoja na Hospitali ya Wilaya itajengwa eneo la Baruti, tutakamilisha miradi hii kabla ya Mwaka 2025 ili wananchi wapate huduma bora,” Alisema Prof. Kitila.

Pia ameongeza kuwa, Rais Samia ameidhinisha Wilaya za Ubungo na Kigamboni kuingia katika miradi ya DMDP ya ujenzi wa barabara ambapo Jimbo la Ubungo limepata Kilomita 55 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 88.5.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania