DRC

Watanzania Milioni 31.2 Kupiga Kura Uchaguzi Wa Serikali Za Mitaa Mwaka 2024

OKTOBA 22, 2024
Border
news image

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais nchini Tqnzania -TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema jumla ya watanzania 31,282,331 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, ambao ni sawa na asilimia 94.83 ya lengo la kuandikisha wapiga kura 32,987,579.

Waziri Mchengerwa ametoa takwimu hiyo ya watanzania waliojiandikisha kupiga kura, wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo ya TAMISEMI.

Mhe.Mchengerwa amesema, takwimu zinaonesha kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 ambapo waliandikishwa wapiga kura 19,681,259 sawa na asilimia 86 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuandikisha wapiga kura 22,916,412.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu nchini Tanzania utafanyika Novemba 27, ambapo jumla ya watanzania 31,282,331 waliojiandikisha ndio wenye haki ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi huo kwa kuchagua wenyeviti wa vijiji, vitongoji, mitaa, wajumbe wa halmashauri ya kijiji pamoja na kamati ya mtaa.

AM/MTV News DRC