TANZANIA

WAKIMBIZU LAKI MOJA KUTOKA BURUNDI KUREJESHWA BURUNDI.

MACHI 27, 2024
Border
news image

Zaidi ya wakimbizi laki moja kutoka nchini Burundi wanaopatiwa hifadhi katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma wametakiwa kurejea nchini mwao kwa hiyari kupitia mpango wa hamasa unaotarajiwa kufikia tamati Desemba 31, 2024. Akizungumza kwa nyakati tofauti na wakimbizi wa nchi hiyo waliopo katika Kambi za Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema mara baada ya kukamilika kwa mpango huo wakimbizi hao watapoteza hadhi ya ukimbizi nchini.

Amesema Mpango huo una lengo la kuhakikisha kila mkimbizi kutoka Burundi anarejea kwa amani, utu na Utulivu kwani kwa sasa nchi hiyo ina usalama na amani hivyo wanapaswa kujitoa katika maisha ya ukimbizi na kwenda kuimarisha uchumi wa Taifa lao. Mh. Andengenye amesema kupitia mpango huo kila mkimbizi atakayerejea nchini kwao atapata dola mia mbili (200) za kimarekani, mgao wa chakula kwa muda wa miezi mitatu sambamba na familia kuondoka na mabati kwa ajili ya kwenda kuanza ujenzi.

"Mpango huu wa hamasa ulianza Januari Mosi, 2024, na unatarajiwa kufikia tamati Desemba 31, 2024 ambapo mashirika yote yanayotoa misaada kwa wakimbizi yatasitisha huduma kufuatia mikataba yao kufikia tamati, hivyo niwasihi mtumie fursa hii itakayowafanya mrudi nchini mwenu kwa hadhi na heshima" amesema Andengenye.

Kwa upande wake, Mratibu wa Idara ya wakimbizi mkoa wa Kigoma Mwita Chacha amewakumbusha wakimbizi hao kutumia muda wa miezi nane uliobaki kuondoka nchini kutokana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) kujielekeza kutoa huduma katika maeneo yenye uhitaji mkubwa hususani yenye machafuko na ukosefu wa amani.

"Nchi ya Burundi kwa sasa ina amani hivyo mashirika ya Umoja wa mataifa yanayotoa huduma kwenu yanaelekeza usaidizi wake kwenye maeneo yenye hali ya ukosefu wa amani kutokana na vita kama Ukraine, Congo DR, Sudani na eneo la Mashariki ya kati" amefafanua Chacha.

"Nchi ya Burundi kwa sasa ina amani hivyo mashirika ya Umoja wa mataifa yanayotoa huduma kwenu yanaelekeza usaidizi wake kwenye maeneo yenye hali ya ukosefu wa amani kutokana na vita kama Ukraine, Congo DR, Sudani na eneo la Mashariki ya kati" amefafanua Chacha.

Tryphone Odas/MTV Tanzania