TANZANIA

"Vifo vya Watoto Wachanga Vimepungua Kanda ya Kati" - RC Senyamule

JANUARI 16, 2024
Border
news image

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma nchini Tanzania Mhe. Rosemary Senyamule amefungua Mkutano wa Afya ya Uzazi na mtoto wa Kanda ya kati katika kupunguza vifo vya kina mama vitokanavyo na Uzazi na vifo vya watoto wachanga unaofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma.

Uzinduzi huo umefanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Jakaya kikwete Jijini Dodoma ambapo amebainisha kupungua kwa vifo vya watoto wachanga na kuwataka waratibu wa Afya ya Uzazi na mtoto wa Wilaya, Mikoa na Kanda kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia vifo vya kina mama vinavyotokana na Uzazi.

"Takwimu zinaonesha kwa Kanda ya kati vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 1929 mwaka 2021 Hadi 1630 Mwaka 2023, vifo vya Uzazi vimeongezeka kutoka 151 mwaka 2021 Hadi vifo 165 mwaka 2023 hivyo mtumie fursa ya Mkutano huu kujadili kwa kina sababu ya vifo hivyo ili kuweka mikakati madhubuti ya kusaidiwa kupunguza vifo hivyo.

"Nachukua fursa hii kuwaomba mtumie Mkutano huu kupanga mikakati kabambe na mahsusi ya kuboresha huduma ikiwemo kusimamia uwajibikaji wa watumishi kwa kuzingatia kauli mbiu ya Mkutano huu 'UONGOZI NA UWAJIBIKAJI NI CHACHU KATIKA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI NA VIFO VYA WATOTO ", amesema Senyamule

Aidha Mhe Senyamule ameweka wazi sababu zinazochangia vifo vya Uzazi ikiwa ni pamoja na kutokwa damu nyingi mara baada ya kujifingua, kifafa cha Mimba, kupasuka kwa Mji wa Uzazi na uambukizo mkali ambapo vifo hivyo vinaweza kuzuilika hivyo ni wajibu wa kikao hicho kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo ili kupunguza na kuzuia vifo vitokanavyo na Uzazi.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma ya Uzazi na mtoto Wizara ya Afya Dkt.Ahmed Makuhani amesema 81% ya vituo vya Afya vina majengo ya kujifungulia, wamefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na Uzazi kwa 80% pia kuhakikisha wanawekeza katika Uzazi wa mpango pamoja na kuhakikisha watoto wa like wenye umri wa Miaka 14 wanapatiwa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa 90%.

Mkutano huo wa Kanda ya kati umewajumuisha waganga wakuu wa mikoa na Wilaya, Wauguzi wakuu wa Mikoa na Wilaya, waratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto, wanafanyakazi wa Sekta ya Afya pamoja na wadau mbalimbali wa Huduma za Afya ya Uzazi na mtoto wa Kanda ya kati ambayo inajumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara pamoja na Wilaya zake zote.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania