TANZANIA

VIFO VYA WANAFUNZI ARUSHA WAZIRI MCHENGERWA ATOA POLE NA AGIZO KWA WAKUU WA WILAYA.

Aprili 14, 2024
Border
news image

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI nchini Tanzania Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaelekeza maafisa elimu nchi nzima kuwaelekeza wakuu wote wa shule na walimu wakuu kwenye maeneo yao kuwaangalia wanafunzi hususani katika kipindi hiki cha mvua ili kuepusha majanga yanayoweza kuepukika.

Waziri mchengerwa ametoa kauli hiyo mapema ikiwa ni siku moja tu tangu kutokea kwa ajali ya gari la shule ya msingi Ghati Memorial Arusha inyodaiwa kusababishwa na ukaidi wa dereva wa gari hilo aliyediriki kukatiza katika mfereji wa maji na kusababisha gari kusombwa na maji hatua iliyo sababisha vifo vya wanafunzi.

Kufuatia ajali hiyo Waziri Mchengerwa ametoa pole kwa shule na familia kufuatia kuondokewa na wanafunzi hao katika mazingira yanayo ashilia uwepo wa uzembe ambao ungeweza kuepukika.

Waziri Mchengerwa amesema katika kipindi hiki cha mvua ni vyema Wakuu wa wilaya wakisisitiza ulinzi wa Watoto kwenye maeneo yao kuanzia kwa maafisa elimu wa wilaya na kata, walimu, wazazi na walezi.

Waziri Mchengerwa ametao kauli hiyo wakati akipokea misaada ya kibinadamu yenye thamani ya Shilingi milioni 70 kutoka kwa Kampuni ya ASAS na Kampuni ya ORYX kwa ajili ya kuwafariji waathirika wa mafuriko wilayani Rufiji Mkoani Pwani.

Misaada hiyo ni Mchele tani 10, Unga wa sembe tani 10,lita 3,000 ya mafuta ya kupikia pamoja na Maziwa lita 1000 Mitungi 300 ya gesi mikubwa na midogo pamoja na majiko yake.

"Kwa niaba ya wananchi wa Rufiji tunawashukuru kwa msaada huu ambao tunaamini unakwenda kuwasaidia waathirika "Amesema Mchengerwa.

Ameongeza kuwa "Sisi Rufiji tuna mafuriko lakini mikoa mingine pia kama Lindi, Arusha na Songwe nayo tunashuhudia inavyo athiriwa na mvua hizi zinazoendelea kunyesha, hivyo niwaombe wasamalia wema tuendelee kuwashika mkono wale wote waliopoteza mali na ndugu katika kipindi hiki kigumu cha mafuriko na tuendelee kuwa watulivu huku tukiliombea taifa kuendelea kushikamana katika shida na raha.

Kwa upande wa Meneja mauzo wa kampuni ya ORYX ,Shaban Fundi pamoja na Meneja mwendeshaji wa kampuni ya ASAS, Abdalatif Ali, wamesema msaada huo ni sehemu ya pole kwa waathirika wa mafuriko Rufiji

MTV Tanzania