Imeelezwa kwamba ukatili wa urembo kwa watoto ni tatizo linalochukua sura mpya kwenye jamii ukiambatana na madhara ya kiafya, kijamii na kisaikolojia.
Hayo yamebainika jijini Dar Es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Sauti ya Watoto Tanzania (SAWATA) yenye lengo la kuelimisha jamii kuhusu kulinda watoto dhidi ya ukatili huo na kutoa maoni juu ya mikakati ya kisera kwa ajili kudhibiti ukatili huo.
Akizungumza na wanahabari Mwenyekiti wa SAWATA Jessica Juma amesema lengo la Taasisi hiyo iliyoanzishwa baadhi ya wananchi ni kupambana na ukatili kwa watoto dhidi ya urembo ili kulinda ustawi na ulinzi wa haki za mtoto iliyo na kaulimbiu isemayo Sauti Yetu, Watoto Wetu.
"Tumejitolea kuungana na Serikali kupaza sauti kwenye jamii katika nyaja ya urembo wenye madhara kwa watoto kwani kumekuwa na ukatili unaoendelea kuwahusu watoto katika nyanja ya urembo" amesema Jessica.
Kwa upande wake Daktari Gasper Shayo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala ametoa wito kwa jamii kuacha kuwalazimisha watoto kufanyiwa urembo hasa unaohusisha kemikali kwani una madhara kwa watoto.
"Kampeni hii itatusaidia pia madaktari kuwaelimisha wananchi, kwani tumekuwa tukipokea wagonjwa mara kadhaa watoto wakiwa wameathirika na bidhaa za urembo zenye kemikali" amesisitiza Dkt. Shayo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizindua Kampeni hiyo, amesema urembo na mapambo hasa ya kemikali yanaweza kuwa na athari mbaya kwa watoto, kiafya, kijamii na kisaikolojia hivyo wazazi na walezi wazingatie hilo ili kumlinda mtoto na athari hizo.
Ameipongeza Taasisi ya SAWATA na kuahidi Wizara itaendelea kushirikiana nao pamoja na wananchi wote wenye ajenda kama hizo kuisadia jamii kuondoka na changamoto mbalimbali zilizopo.
Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza kwamba athari za ukatili wa urembo ni pamoja na watoto kutojiamini kuhusu muonekano wao, maambukizi ya ngozi, watoto kujitenga wanapokosa urembo na kushindwa kutambua tofauti ya urembo halisi na ule wa mapambo.
"Kwa kuzingatia athari hizo ni dhahiri kuwa kampeni hii ni muhimu sana katika kuhakikisha watoto wa Tanzania wanakua na kujenga maisha yao bila kudhurika kisaikolojia au kimwili kutokana na masuala ya urembo". Amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima.