TANZANIA

TARIME WATAKIWA KUANZA KUTUMIA JENGO LA KITUO JUMUISHI

Aprili 05, 2024
Border
news image

Mkurugenzi wa huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI nchini Tanzania Dkt. Rashid Mfaume ametoa muda wa wiki moja kwa Halmashauri ya Tarime kukamilisha na kuanza kutumika kwa jengo la kituo jumuishi linalojengwa katika Hospitali ya Halmashauri hiyo.

Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo baada ya kukagua ujenzi wa jengo hilo ambalo lilianza kujengwa mwaka 2022 kwa mkataba wa miezi mitatu likigharimu kiasi cha shilingi milioni 117 zilizotolewa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi ya Watu (UNFPA).

“Mkataba wa kazi hii mpaka ukamilike ulikuwa ni wa miezi mitatu sasa ukiangalia zaidi ya mwaka umepita na kajengo kenyewe ni kadogo na tunaathiri wananchi ambao wanapata kadhia ya ukatili wa kijinsia na ukatili wa watoto kwasababu ya urasimu wa watumishi wa serikali”

Katika kuhakikisha jengo hilo linakamilika na kuanza kutumika Dkt. Mfaume amemuelekeza mganga mkuu wa mkoa kumuomba katibu Tawala wa mkoa Mara kupeleka timu ya kuchunguza thamani ya matumizi ya fedha katika ujenzi huo.

Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya hiyo Dkt. Joseph Mzigu amekiri kupokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.

Timu ya Afya,Ustawi wa jamii na Lishe kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI ikiongozwa na mkurugenzi Dkt.Rashid Mfaume ipo mkoa wa Mara kwa ziara ya kukagua shughuli za uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Afya katika mkoa huo.

MTV Tanzania