Serikali ya Tanzania imelitaka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuweka usawa kwenye kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoendelea kutoka Duniani na kuziwesha nchi zinazoendelea kupata fursa sawa za uwekezaji wa viwanda vya dawa, chanjo, vifaa na vifaatiba, pamoja na misaada ya rasilimali kwenye kukabiliana na majanga.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya nchini Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha Tamko la Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kikao cha Azimio la Kukabiliana na majanga na dharura kilichofanyika kwenye Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa Jijini New York.
Waziri Ummy amesema kuwa nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania imejifunza mengi kupitia mlipuko wa Ugonjwa wa UVIKO-19 na namna ulivyoleta athari mbalimbali ndani ya jamii, hivyo sasa ni nyema kuwa na mikakati endelevu yenye usawa katika kukabiliana majanga.
"Kama nchi moja haipo salama, basi sote hatupo salama, tunahitaji kuona mabadiliko ya usawa wa kupambana na majanga na kuwa na maazimio yenye kuleta usawa kwenye mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko na dharura za masuala ya afya" amesisigiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania ilipatwa na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg mnamo mwezi wa tatu, na katika kipindi cha miezi 3 ilifanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambao ulitokea Mkoani Kagera.
Ametaja mkakati mojawapo wa kuongeza usalama wa masuala ya afya ni kupitia Watoa Huduma za Afya ngazi ya Jamii ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za afya ngazi ya msingi.