TANZANIA

TANZANIA KUJENGWA MTAMBO MKUBWA WA UCHENJUAJI MADINI YA KINYWE UTAKAOZALISHA TANI 500 HADI 600 KWA SIKU

FEBRUARI 06, 2024
Border
news image

Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya Kinywe (Graphite) katika mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa wa Tanga ,Lindi na Morogoro.

Uwekezaji katika sekta ya madini nchini unaendelea kukua kwa kasi ambapo kwasasa Tanzania inatarajia kuwa na mtambo mkubwa wa uzalishaji madini kinywe unaojengwa na Kampuni ya GodMwanga Gems Limited mkoani Tanga.

Akielezea maendeleo ya ufungaji wa mtambo meneja uzalishaji katika Mgodi huo Henry Mbando alimwelezea Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa juu ya ubora wa mtambo wa kuchenjua madini hayo, kuwa mtambo huo utachenjua madini kutoka katika miamba na utazalisha kiasi cha tani 500 - 600 kwa siku.

Mbando alifafanua kuwa mtambo unaofungwa una uwezo wa kusaga tani 6000 za mwamba wa madini ya kinywe na utachenjua ili kupata ubora wenye asilimia 97 ya madini ya kinywe.

Akielezea juu ya mpango wa ulipaji kodi kupitia uzalishaji huo Mbando alifafanua kuwa ulipaji wa kodi kwa mwezi utafanyika kulingana uzalishaji ambapo asilimia tatu ya kodi ya mrabaha itakuwa kiasi cha Tshs.546,000,000, asilimia moja ya kodi ya ukaguzi itakuwa Tshs.182,000,000 na kodi ya service levy yenye asilimia sifuri nukta tatu itakuwa Tshs 54,600,000.

Kuhusu mchango wa kampuni kwa jamii (CSR) Mbando alisema mpaka sasa tayari ujenzi wa zahanati na nyumba ya mganga wenye thamani ya Tshs.200,000,000 umefanyika.

Changamoto kubwa ya mradi huo iliyotolewa na uongozi wa mgodi ni kukosekana kwa nishati ya umeme ya uhakika na ubovu wa miundombinu ya barabara ambapo uongozi umeiomba serikali kuwasaidia.

MTV Tanzania