Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Mohammed Mchengerwa amekemea vitendo vya baadhi ya wakuu wa shule wanaokataa kuwapokea watoto kwasababu hawajachangia fedha za michango ya shule ile hali tayari serikali imeshawalipia watoto wote gharama za shule na elimu ya Tanzania utolewa bure.
Huku akiagiza watoto wote wenye sifa za kusoma wapokelewe shule bila masharti yeyote ya michango kwani tayari serikali imeshalipia na kila mwezi zinatoka zaidi ya Shilingi Bilioni 2 kwaajili yakugharamia wanafunzi mashuleni na atakayeshindwa kutekeleza maagizo hayo atachukuliwa hatua kwa kuwekwa kando kwani hatoshi kwenye eneo lake pamoja na afisa elimu anayemsimamia.
Mhe.Mchengerwa amekemea tabia hiyo Wilayani Chalinze mkoani Pwani wakati akisikiliza na kutatua changamoto za wananchi ambapo baadhi ya wananchi waliibua hoja ya wanafunzi kukataliwa shuleni kutokana na kukosa baadhi ya michango iliyowekwa na shule mbalimbali kinyume na masharti ya serikali yakuagiza elimu itolewe bure.
Katika hatua nyingine Mhe.Mchengerwa amewaagiza Wakuu wa mikoa kukaa mguu pande kwa kutatua changamoto za wananchi wanazoziibua katika mikutano ya adhara inayofanywa na baadhi ya viongozi pindi wanapofika katika maeneo yao na kwa ambaye hataweza kutekeleza maagizo ya chama niwazi hawezi kuwahudumia wananchi.