TANZANIA

Silaa Ataka Kliniki za Ardhi Zitende Haki Sawa

JANUARI 20, 2024
Border
news image

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania Mhe. Jerry Silaa amesema ataleta Kliniki ya Ardhi katika wilaya ya Kinondoni itakayosimamiwa na viongozi wa kitaifa ili kushughulikia na kutatua migogoro ya ardhi ya wilaya hiyo ambayo imekuwa kinara wa migogoro nchini.

Waziri Silaa ametoa ahadi hiyo wakati alipofika katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Bunju A vilivyopo Kata ya Bunju wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es salaam ambapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda alitoa wito wa kumtaka Waziri Silaa afike eneo hilo na kushughulikia migogoro ya ardhi haraka.

Katika kutekeleza maelekezo hayo Waziri Silaa amesema kuanzia tarehe 19 Februari 2024 ataleta Kiliniki ya ardhi ya aina yake ambayo yeye na viongozi wote wa Kitaifa, Mkoa wa Dar es salaam na Wilaya ya Kinondoni wanaohusika na sekta ya ardhi watashiriki Kliniki hiyo.

Aidha, Silaa ameipa jina Kliniki hii kama ni Kliniki ya Kitaifa kwa kuwa itahusisha viongozi wote wakuu wa Wizara yake ambao ni Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Kamishna wa Ardhi na viongozi wengine watapiga kambi eneo la viwanja vya Shule ya Msingi ya Bunju A.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania