TANZANIA

Serikali Ya Tanzania Kuanza Kuzalisha Umeme Wa Jotoardhi 2025

JANUARI 20, 2024
Border
news image

Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ya umeme itokanayo na nishati ya Jotoardhi katika maeneo mbalimbali nchini kupitia Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga jijini Dodoma wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Rasilimali ya Jotoardhi iliyofanyika.

Miradi ya kuzalisha umeme kutokana na Jotoardhi inayoendelea kutekelezwa nchini ni Ngozi 70MW na Kiejo - Mbaka 60MW iliyopo Mbeya, Sogwe 5MW, Luhoi 5MW mkoani Pwani na Natron 60MW uliopo Arusha.

"Kati ya miradi hiyo mitano, miradi minne ipo katika hatua ya uhakiki wa rasimali ya Jotoardhi na mradi mmoja wa Natron upo katika hatua ya utafiti wa kisayansi wa kina," amesema Naibu Waziri Kapinga.

Amesisitiza kuwa suala la sheria ya Uendelezaji miradi ya Jotoardhi litafanyiwa kazi na Serikali ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2025/2026 kuwe na uzalishaji wa Megawati 30 kutokana na umeme wa Jotoardhi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Mathayo David Mathayo amepongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme inayotokana na Jotoardhi.

Semina hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga na Watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Uendelezaji ya Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania