TANZANIA

SERIKALI INATAMBUA UMUHIMU WA DINI NA TAASISI ZA KIDINI-RC SENYAMULE

FEBRUARI 21, 2024
Border
news image

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa tamko hilo alipofanya ufuatiliaji wa Taasisi ya Ally-Habshi inayojishughulisha kutoa mafundisho ya Madrasa kufuatia kukamatwa kwa Mwalimu wake Bw. Yusuph Mohamed kwa tuhuma za kukutwa akitoa mafundisho ya Dini kwa watoto 132 kwenye mazingira hatarishi yasiyo na huduma muhimu za Kijamii.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kituo cha kulelea watoto wenye uhitaji kilichopo Kata ya Kikombo Jijini Dodoma ambacho ndicho watoto hao walipelekwa baada ya kutolewa kwenye maeneo waliyokutwa Mtaa wa Sogeambele na Nkuhungu kufuatia kukamatwa kwa Mwalimu wao.

Mhe. Senyamule amesema Serikali inatambua umuhimu wa Dini,Taasisi za Dini na nafasi ya viongozi wa Dini zote katika kujenga kizazi chenye hofu ya Mungu na kuwa na maadili mema.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Mafunzo ya Dini kwa watoto ni jambo lenye umuhimu mkubwa na linaugwa mkono na Serikali kwani Mkoa unashirikiana kwa Karibu na viongozi wa dini katika mikakati mbali mbali ya maendeleo ya Mkoa.

“Taasisi ni lazima kabla ya kuanzishwa, ifuate vigezo vyote vinavyotakiwa vya kijamii, naelekeza usajili na uendeshaji wa makao ya watoto ufuate utaratibu.

“Taarifa ya awali ya ukaguzi wa miundombunu ya Taasisi hii imebainisha ukiukwaji wa sheria. Viongozi wa mitaa na vijiji hakikisheni munatambua wageni wote wanaoingia katika maeneo ya utawala pamoja na kufuatilia shughuli wanazozifanya” Amesema Mhe. Senyamule.

Tukio hilo lilitokea Februari Pili 2024 wakati Timu ya Mkoa ilipofika katika vituo vya Taasisi hiyo vilivyopo maeneo ya Nkuhungu na Chihanga baada ya kupata taarifa ya uwepo wa vituo hivyo na kubaini baadhi ya watoto ambao wametoka Dodoma na mikoa ya jirani kama vile Arusha na Manyara kupatiwa mafunzo hayo.

MTV Tanzania