TANZANIA

SERIKALI ZA VIJIJI ZISHIRIKISHWE KATIKA KULEA VITUO VYA MALEZI NA MAKUZI YA MTOTO

Aprili 10, 2024
Border
news image

Mkurugenzi Msaidizi huduma za Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais -TAMISEMI nchini Tanzania Bi. Subsiya Kabuje amevitaka Vituo vya Malezi na Makuzi ya Mtoto kuhakikisha vinashirikisha viongozi wa Serikali ya Kijiji katika kulea vituo hivyo vinavyomilikiwa na jamii.

Ameeleza hayo ikiwa ni muendelezo wa ziara akiwa ameambatana na wataalum kutoka TAMISEMI, Wizara Maendeleo ya Jamii, na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ya kukagua vituo vya malezi na makuzi ya watoto katika Halmashuri ya Wilaya Chamwino mkoani Dodoma.

Bi. Kabuje amesema Serikali ya Kijiji ikishirilishwa ipasavyo itasaidia kuangalia na kusimamia vituo ambavyo vimejengwa katika shule za msingi vikiwa na lengo la kuwarahisishia watoto wa eneo husika kuzoea mazingira ya shule.

Pia ameongeza kwa ushirikiano huo ukiwa madhubuti itakua rahisi kwa pamoja kuangalia namna ya kushirikiana kutunga sheria ya kuwaongoza katika kuchangia chakula cha watoto wanaolelewa katika vituo hivyo.

Aliongeza kuwa azma ya Serikali ni kuendeleza vituo hivyo hasa katika kuangalia malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika kumjengea maadili mazuri na kumuepusha na changamoto zinazoweza kuzuilika hasa katika suala la kuzuia vitendo vya ukatili.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Chamwino Ikulu Peter Simba amesema wataendelea kusimamia vituo hivyo sababu vinamanufaa kwa watoto na wazazi huku akishauri Serikali kuangalia wa kuwalipa posho walezi wanaosimamia vituo hivyo ili wawe na ari ya kuendelea kuvisimamia na kutoa huduma kwa watoto.

MTV Tanzania