TANZANIA

Serikali ya Tanzania imesema meli iliyo zama ziwa tanganyika ni mali ya serekali ya Congo

Aprili 09, 2024
Border
news image

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limesema meli iitwayo MV Maman Benita, iliyozama katika eneo la Kabimba, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) ni mali ya kampuni kutoka nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na TASAC, leo April 8, 2024; imesema meli hiyo imesajiliwa chini ya bendera ya DRC na inamilikiwa na kampuni ya Kikongo, iitwayo Établissement Manimani.

Kabla ya kuzama kwa meli hiyo katika Ziwa Tanganyika, ilianza safari yake Aprili 6, 2024 saa 12:00 jioni ikitokea bandari ya Kigoma kuelekea Kalemie, DRC; ikiwa imebeba jumla ya abiria 27.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, abiria hao ni pamoja na Watanzania watano, raia wa China wanne, raia wa Kongo kumi na sita, raia mmoja wa Kenya pamoja na mtoto mdogo.

Meli hiyo iliyotarajiwa kuwasili Kalemie majira ya saa 8:00 usiku, hata hivyo haikufika, ambapo asubuhi ya Aprili 7, 2024, wavuvi walifanikiwa kumwokoa abiria mmoja mwenye asili ya China, na kisha kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali ya DRC, juu ya kuzama kwa meli hiyo ya MV Maman Benita.

Baada ya kupata taarifa hiyo, zoezi la utafutaji na uokoaji lilianza mara moja ambapo hadi kufikia majira ya saa 1:00 usiku wa April 7, 2024, waathrika 17 walikuwa wameshaokolewa, kati yao ikijumuisha Wachina 2, Watanzania 3, na Wakongo 12.

Aidha, chanzo cha kuzama kwa meli bado hakijajulikana isipokuwa Nahodha wa meli hiyo ameokolewa na timu ya wataalam tayari imekwenda eneo la tukio kwa ajili ya ufuatiliaji. Zoezi la utafutaji kuokoa abiria waliosalia linaendelea.

TASAC inaendelea kutoa rai kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo majini kuzingatia Sheria na Kanuni za udhibiti usafiri majini na kuhakikisha chombo kina kuwa na majaketi okozi ya kutosha na kwa vyombo vidogo kuhakikisha abiria wanavaa jaketi okozi wakati wote wa safari ili kujiepusha na maafa yanayoweza kusababishwa na tukio la ajali.

Aidha, TASAC inatoa pole kwa waathirika pamoja na familia kwa ujumla na taarifa kamili juu ya ajali hii itatolewa.

MTV Tanzania