TANZANIA

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kusimamia usawa wa mgawanyo wa fedha za Mfuko wa Jimbo kwa kuzingatia Sheria ya Mfuko wa Jimbo ambayo inatumika Tanzania Bara na Zanzibar.

JANUARI 30, 2024
Border
news image

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameiarifu Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria jijini Dodoma.

Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25, ametaja vigezo viliyowekwa katika Sheria hiyo ni asilimia 25 ya fedha hugawanywa sawa kwa idadi ya majimbo yote.

Mhe. Dkt. Jafo amesema kuwa asilimia 10 ya fedha za Mfuko wa Jimbo hugawanywa kulingana na ukubwa wa eneo wakati asilimia 20 hugawanywa kulingana na kiwango cha umaskini.

Halikadhalika, Waziri Dkt. Jafo amefafanua kuwa Mfuko huo wenye lengo la kuchochea maendeleo ya majimbo ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, asilimia 45 hugawanywa kulingana na idadi ya watu.

Aidha, amewashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa ushauri walioutoa kwa Ofisi ya Makamu wa Rais ambao umesaidia katika mafanikio na kuahidi kuendelea utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Florent Kyombo ameahidi kamati hiyo itaendelea kuisimamia vyema Ofisi ya Makamu wa Rais ili malengo mahsusi ya kazi yatimie.

MTV Tanzania