Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania Mhe. Mohamed Mchengerwa amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wananchi wa Rufiji kwa miradi mingi iliyotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza leo msafara wa Mhe. Rais Samia aliposimama kuwasalimia wananchi wa Rufiji kwenye eneo la Ikwiriri wilayani humo, Mhe. Mchengerwa amesema hapo awali wananchi wa Rufiji walikuwa kama wametengwa kwa kutopatiwa miradi yenye kuwaondolea adha ya kupata huduma bora.
“Hatukuwa na vituo vya afya vya kutosha kulikuwa na upungufu mkubwa wa Shule za Msingi na Sekondari, miundombinu duni ya barabara sambamba na madaraja ambapo hapakuwa na mawasiliano, ila kwa kipindi hiki cha miaka miwili ambayo Mhe. Rais Samia upo madarakani kila Tarafa katika Wilaya hiyo imepata Kituo cha Afya na kwa sasa changamoto hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa.”
“Na zaidi katika eneo la Afya tumepata kiasi cha sh.Milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali Kongwe ya Wilaya na zaidi kupitia fedha za CSR nimejulishwa kuwa tutapatiwa sh. Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali Mpya ya Wilaya hakuna zaidi cha kusema ila tunakushukuru,”amesema.
Amebainisha kuwa elimu ya watoto wa Rufiji imeimarika sana kwa kuatiwa fedha za ujenzi wa shule za Msingi za kutosha pamoja na Sekondari na kwa sasa wanajenga shule nyingine ya Wasichana ya Bibititi Mohamed.
“Sisi wana Rufiji tumejawa na moyo wa shukrani kwa yote uliyotufanyia Mhe. Rais hapa Ikwiriri utaona taa nyingi za barabarani ambazo zinapendezesha Mji wetu na kuongeza ulinzi na sasa tunakushukuru kwa kuridhia barabara ya Nyamwage - Utete kujengwa kwa kiwango cha Lami pamoja na Daraja la Mbande tunakushkuru sana Mhe. Rais.”amesema.
Kadhalika, amesema Rais ameridhia ombi la muda mrefu la ujenzi wa barabara ya Ikwiriri kwenda Mkongo kwa kiwango cha lami pamoja na daraja la Muhoro ambao ujenzi utaanza mwezi Oktoba mwaka huu.
Mhe. Rais akiwa safarini kutoka Lindi baada ya ziara ya kikazi amesimama na kusalimia wananchi wa Somanga, Rufiji, Kibiti pamoja na kuzindua kiwanda cha uzalishaji vioo vya ujenzi cha Sapphire Float Glass kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.