TANZANIA

RRH Zashauriwa Kufanya Maboresho Kama Muhimbili Tanzania

OKTOBA 04, 2023
Border
news image

Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya nchini Tanzania wameshauriwa kuiga mfano wa maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa lengo la kuboresha hospitali hizo zaidi ya ilivyo sasa.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi katika kikao maalumu na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Temeke, Amana, Mwananyamala, Waganga Wakuu wa Manispaa hizo, Kamishna Msaidizi wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai (Forensic Bureau), Msaidizi wa Kamishna Mkuu wa Upelelezi-Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa Mkoa huo ili kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano.

Prof. Janabi amesema kuwa kuna maboresho ambayo si lazima kujenga majengo mapya kwani mengine yanahitaji ukarabati hivyo ni muhimu sana Viongozi hao kujifunza MNH imefanyaje kuboresha miundombinu na hali ya utoaji huduma ili kuweza kuboresha maeneo yao.

Amewashauri kudhibiti mianya na upotevu wa fedha, kusimamia watumishi vizuri ili waweze kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa wagonjwa waliolazwa, upasuaji, wagonjwa wa nje na huduma za vipimo mbalimbali vya uchunguzi.

Prof. Janabi amewahakikishia Waganga Wafawidhi wa RRH kuwa MNH ipo tayari kushirikiana nao ili kubadilishana ujuzi kupitia tiba mtandao hususani kupitia vifaa tiba vilivyofungwa katika Hospitali hizo kupitia fedha za IMF.

Viongozi hao kwa pamoja wameupongeza Uongozi wa MNH kwa kazi kubwa iliyofanyika chini ya Prof. Mohamed Janabi na wameongeza kuwa kuna mengi wanajifunza kila siku kutokana na maboresho yaliyofanyika.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania