Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuwa shughuli zote za uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 pamoja na Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 zitaendelea kama ilivyokuwa awali kwa kuzingatia taratibu na mipaka ya vijiji na vitongoji iliyokuwepo awali kwenye maeneo yao.
Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi kwaniaba ya Mhe. Rais Samia, ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 23, 2024 alipozungumza na mamia ya wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro, akiagiza pia askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutowanyanyasa wananchi pamoja na kuheshimu mamlaka za serikali za mitaa zilizopo kwani Mhe. Rais Samia bado anatambua uwepo wa serikali za vijiji na vitongoji vya maeneo hayo.
Kwa upande wake Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda mbali ya kuwashukuru wananchi kwa uvumilivu na imani yao kwa serikali, amemuhakikishia Waziri Lukuvi kuwa atasimamia maelekezo yote yaliyotolewa kwake, akiahidi pia kuhakikisha huduma zote za kijamii zilizokuwa zimesimama ama kusuasua hasa katika sekta ya afya na Elimu zinarejea katika ubora wake na kwa viwango vinavyohitajika.
Katika ziara hiyo, Mhe. Lukuvi ameambatana na Mhe.Prof. Palamagamba Kabudi Waziri wa Katiba na sheria, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula pamoja na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania CP Awadh Juma Haji pamoja na Viongozi wengine wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi CCM.