Madaktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Chakula Ini na Kongosho wa Hospitali ya Taifa Muhimbili nchini Tanzania (MNH) wamemfanyia upasuaji mgonjwa mwenye umri wa miaka 48 na kutoa mawe 62 yaliyokuwa kwenye mfuko wa nyongo ikiwa ni mara ya kwanza kutoa mawe mengi kwa mgonjwa.
Akizungumza kwa niaba ya jopo lililoshiriki kufanya upasuaji huo, Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji Mfumo wa Chakula, Ini na Kongosho, Dk. John Ngendahayo, amesema mgonjwa huyo alikuja hospitalini hapo akiwa na maumivu makali na mwili uliodhoofika baada ya kupewa rufaa kutoka Mbeya akiwa na dalili mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa manjano, kuwashwa mwili mzima ambao ulimfanya ajikune mwili na kumsababishia vidonda.
“Mgonjwa alikuwa hajui ana mawe kwenye mfuko wa nyongo kwakuwa alikuwa na dalili mbalimbali ila baada ya kumfanyia kipimo cha CT-Scan kilionyesha mfuko wa nyongo ulikuwa umeathirika kwa sababu mawe yalikuwa mengi na nyama za tumbo kushikana hivyo tulishauriana na wataalamu kumfanyia upasuaji ili kutoa mawe uliochukua saa nne,” amesema Dk. Ngendahayo.
Amesema sababu zinazosababisha mtu kupata mawe kwenye mfuko wa nyongo kuwa ni nyongo kupata mgandamizo ndani ya mfuko wa nyongo na kujiongeza uzito kutokana na madini ya chumvi au mafuta mwilini (rehemu) ambayo hutengeneza ujiuji na baadaye kuganda na kutengeneza mawe na mawe hayo baadaye huyeyuka ila kuna mengine ambayo huwa hayayeyuki.
Amesema mtu anaweza kuishi na mawe hayo bila kujua ila baadaye yanaweza kumsababishia kupata maumivu makali tumboni hasa upande wa kulia chini ya mbavu, kupata manjano, mwili kuwasha kiasi cha kukosa usingizi, kupata kichefuchefu, kukosa hamu ya kula na dalili nyingine kama hizo.
Dk Ngendahayo ametoa wito kwa jamii kuwa na utamaduni wa kwenda hospitali kufanya uchunguzi wa afya hasa pale wanapohisi kuwa na maumivu kwenye tumbo au wanapopata manjano.
Amesema mgonjwa huyo anaendelea vizuri .