TANZANIA

MTO NYALI-NZUMBO KUJENGWA DARAJA LA KUDUMU LA CHUMA

JANUARI 29, 2024
Border
news image

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini nchini Tanzania(TARURA) inatarajia kuanza usanifu wa daraja la kudumu la chuma (Mabey Bridge) litakalojengwa ili kuunganisha vijiji vya Nyali na Nzumbo katika kata ya Ulaya-Mikumi Wilayani Kilosa Morogoro.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff wakati akiongea na wananchi wa kata hiyo kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya miundombinu wilayani Kilosa.

“Nitawatuma wataalamu wangu wa TARURA Makao Makuu waje wafanye usanifu wa ujenzi wa daraja la kudumu la chuma ili kuunganisha vijiji hivi vya Nyali na Nzumbo”. Alisema

Pamoja na hilo, amemwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro kuanza mara moja ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu(Kiteputepu)ili wananchi wa vijiji hivyo waendelee kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Vile vile Mhandisi Seff ameelekeza kufanyika kwa tathimini ya uharibifu wa barabara za Mikumi ili ziwekwe kwenye mpango wa dharura wa kurudisha mawasiliano haraka iwezekanavyo.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Mikumi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge - TAMISEMI Mhe. Dennis Londo amesema barabara nyingi za Jimbo la Mikumi zimeharibika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuiomba TARURA kuangalia uwezekano wa kukarabati hasa barabara za Kivungu-Kilangali Km. 1.5, barabara ya Miyombo-Dodoma Isanga Km. 10 pamoja na ujenzi wa daraja la kudumu la Nyali-Nzumbo.

Daraja la watembea kwa miguu katika mto Nyali ambalo linaunganisha vijiji vya Nyali na Nzumbo litajengwa kufuatia lile la awali kuvunjika.

MTV Tanzania