TANZANIA

Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewahimzia wawekezaji wa migodi nchini kuhakikisha wanakuwa na mtaalamu wa mazingira

JANUARI 20, 2024
Border
news image

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira Tanzania) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewahimzia wawekezaji wa migodi nchini kuhakikisha wanakuwa na mtaalamu wa mazingira ili wawashauri namna bora ya kulinda mazingira.

Amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 kwenye kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Anglo De Beers kilichopo Mwaoga Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Akitembelea bwawa la tope sumu (TSF) katika kiwanda hicho ambalo limejengwa kwa matumizi ya mwaka mmoja, Dkt. Jafo amempongeza mwekezaji huyo kwa kuwa ameanza kujenga miundombinu ya uhifadhi mazingira kabla kuanza kwa shughuli za uchimbaji kama sheria na kanuni zake zinavyoelekeza.

“Nimetembelea kiwanda hiki cha kuchenjua dhahabu na nimeridhishwa na namna mlivyojipanga katika uzalishaji wa madini hayo hasa nimeona bwawa la tope sumu ambalo mtahifadhi majitaka, tunataka wengine waige mfano huu,“ amesema.

Aidha, Waziri Jafo ametembelea eneo la uzalishaji ambapo mitambo yote inayotumika katima uchhenjuaji wa dhahabu imesimikwa kwa maandalizi ya uzalishaji kwa kuwa ameshatimiza masharti yote ya uhifadhi wa mazingira ikiwemo mchakato wa uandaaji wa eia.

Amesema Serikali inahamasisha uwekezaji ukiwemo wa madini lakini wawekezaji hao pamoja na kuwa na mtu wa kusimamia usalama wa wafanyakazi wanapaswa pia kuzingatia kulinda mazingira.

Dkt. Jafo ameongeza kuwa sema uwekezaji ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu lakini unapaswa kulinda mazingira kuepuka madhara ya kiafya yanayoweza kuwapata wananchi hususan wale wanaozunguka miradi hiyo ikiwemo ya uchimbaji wa dhahabu.

Pia, amesisitiza wachimbaji kuwa na mabwawa ya tope sumu (TSF) ambayo yana kazi ya kuhifadhi majitaka ili yasisambae ovyo katika makazi ya wananchi kupitia mito midogo midogo na kuleta madhara ya kiafya.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera amesema Serikali ya mkoa huo inaendelea kutoa ushirikiano na wawekazaji ili kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa kufuata matakwa ya sheria.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania