Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania Mhe.Mohamed Mchengerwa ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) katika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo kwenye kikao chake na Mwakilishi Mkaazi wa Benki ya Dunia Bw. Natham Belete pamoja na Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Tanzania Bi. Elke Wisch.
Amesema kupitia benki hiyo wamekubaliana utekelezaji wa haraka wa miradi mbalimbali hususani wa Bonde ya Mto Msimbazi ambako litajengwa daraja la juu la kisasa na miundombinu ya kuzuia mafuriko.
"Mradi huu mkubwa utahusisha ujenzi wa daraja hilo la kisasa, kujaza kifusi pamoja na kupendezesha eneo hilo la Msimbazi kuwa na mandhari nzuri ya kupumzikia kwa wakazi wa mkoa wa Dar es salaam,"amesema.
Waziri huyo amesema kikao hicho kimelenga kujadili namna gani watapiga hatua katika mradi huo ili utekelezaji uanze mara moja kwa kushirikiana na wadau pamoja na Wizara mbalimbali zinazohusika.
"Ile dhamira na maono aliyonayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anaijenga na kuiboresha Miji yetu tutatimiza ndoto zake ili kuleta utulivu kwa watanzania kwa kutumia miundombinu bora na kwa kujali afya za watoto wetu,"amesema.
Kuhusu UNICEF, Mhe. Mchengerwa amesema wamethibitisha kuwa na fedha za kutekeleza miradi ya afya, lishe na malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
"Niwaahidi ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza yale yote tuliyokubaliana na kwa chochote kitakachokwamisha tuwasiliane mapema ili tuweze kuchukua hatua za haraka na kazi ya kupeleka huduma bora kwa wananchi iendelee," amesema.