TANZANIA

Mazingira ya Biashara Yaimarika Tanzania - Dkt. Mpango

FEBRUARI 27, 2024
Border
news image

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Awamu ya Sita, mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji yameimarika na kuwa bora zaidi kwa kipindi kifupi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa mwaka 2024 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha uwekezaji na nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara licha ya misukosuko ya uchumi na kijamii inayoendelea Duniani kote. Ameongeza kwamba katika mwaka 2023, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kuwa 5.0% ikilinganishwa na 4.7% mwaka 2022 huku matarajio kwa mwaka 2024 ni ukuaji wa 5.5%.

Makamu wa Rais amewasihi washiriki wa Jukwaa hilo kutoa maoni na mapendekezo kwa uhuru ili kuweza kuboresha vema sera za kodi na uwekezaji nchini. Amesema maoni yatakayotolewa katika Jukwaa hilo yatatumika katika mchakato wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025. Aidha amewataka Mawaziri wa Fedha kuzingatia ushauri wa sekta binafsi na walipa kodi wote ili wadau waone umuhimu wa ushiriki wao katika jukwaa hilo.

Halikadhalika ametoa wito kwa washiriki kujikita katika kuibua njia za kibunifu zitakazosaidia kuongeza mapato ya Serikali bila kuumiza Wafanyabiashara na Wawekezaji. Amewataka kujadiliana kwa kina kuhusu namna ya kutumia zaidi ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, mathalan kupitia hatifungani zitakazotolewa na taasisi na mashirika ya umma kugharamia miradi ya maendeleo. Pia amewasihi mijadala kujielekeza katika kubaini na kudhibiti vihatarishi vya matumizi ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, ikiwemo wizi wa kimtandao na utoroshaji wa mitaji.

Makamu wa Rais amesema tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani imeendelea kufanya maboresho ya sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa kodi ili kujibu malalamiko ya Wawekezaji ikiwemo Kurekebisha sheria za kodi, Kuweka utulivu wa sera za kodi, Kuendelea kujenga na kuimarisha vituo jumuishi vya huduma za uwekezaji na biashara ikijumuisha ujenzi wa vituo 10 vya utoaji huduma kwa pamoja mipakani (One-Stop Border Posts), Kufanya mapitio na kuhuisha sera na sheria mbalimbali pamoja na Kukamilisha Mfumo wa Dirisha Moja la Kutoa Huduma kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuunganisha mifumo ya taasisi saba (7) ambazo ni NIDA, TRA, BRELA, TIC, Kazi, Uhamiaji na Ardhi.

Pia amesema hatua zingine zilizochukuliwa ni pamoja na Kuanzisha Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko ya Walipakodi, kuwianisha majukumu ya kitaasisi ili kurahisisha utoaji huduma, Kuendelea kufanya mashauriano baina ya Serikali na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara pamoja na kutoa vivutio vya kikodi ikiwemo kutoa misamaha ya kodi na kiwango cha asilimia sifuri (0) cha ushuru wa forodha kwa bidhaa mtaji na malighafi.

Makamu wa Rais amesema makusanyo ya mapato ya Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita yaliongezeka kwa 22.1% kutoka Sh. trilioni 17.6 mwaka 2020/21 hadi Sh. trilioni 22.6 mwaka 2022/23. Ongezeko hilo la ukusanyaji wa mapato limeiwezesha Serikali kuendelea kuongeza Bajeti yake kutoka Sh. trilioni 36 mwaka 2021/22 hadi Sh. trilioni 44.4 mwaka 2023/24.

Amesema Ongezeko la bajeti limewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na injini na mabehewa yake, mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (94.8%, mradi wa Kinyerezi I Extension (100%) na mradi wa kufua Umeme wa Maji Rusumo (99.7%). Vilevile kupeleka huduma ya umeme kwenye vijiji 10,987 kati ya vijiji 12,318 vya Tanzania Bara (sawa na 89.19%), ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara na madaraja unaendelea ambapo jumla ya miradi 23 ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na daraja la Kigongo - Busisi (80.0%).

MTV Tanzania