Tanzania

Makamu rais mhe dkt mpango aanza ziara ya kikazi mkoani kigoma

JULAI 09, 2024
Border
news image

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameuelekeza Uongozi wa Serikali Mkoani Kigoma kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wa Umma wasio waadilifu wanaoruhusu uingizwaji holela wa mifugo katika wilaya ya Uvinza hali inayochochea migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Akizungumza na wakazi wa wilaya ya Uvinza, Dkt.Mpango amesema baadhi ya watumishi wa Umma wasio waadilifu wamekuwa wakipokea fedha kinyume na sheria ili kuwaruhusu wafugaji kuingiza mifugo yao wilayani humo kwa ajili ya kufuata malisho bila kufuata utaratibu.

"Mamlaka za vijiji zinapaswa kuzingatia Sheria na Kanuni za matumizi bora ya Ardhi, hivyo nakuagiza Mkuu wa Mkoa kwa kushirikia na watendaji wako kutosita kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanaovunja sheria na maelekezo ya Serikali kwa kushindwa kufuata taratibu za ufugaji kwani nchi hii haitegemei mifugo pekee" amesema Dkt. Mpango.

Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa Barabara ya Malagarasi, Ilunde hadi Uvinza yenye urefu wa Km51.1 ambayo ujenzi wake umefikia 54 % na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 2025.

Mara baada ya kukagua mradi huo, Mhe Dkt. Mpango amemshauri Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha

anatumia kipindi hiki cha kiangazi kukamilisha maeneo muhimu ya ujenzi wa barabara hiyo bila kuathiri ubora wa kazi.

Amesema lazima barabara zikamilike kwa wakati ili kutimiza azma ya Mhe. Rais ya kutaka kuufungua mkoa wa Kigoma ili uweze kuwa Kitovu cha biashara na Uchumi kwa Ukanda wa Magharibi.

Aidha kupitia ziara hiyo Dkt. Mpango amekagua na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa vituo vya kupoza umeme KV 132 kilichopo Nguruka wilayani Uvinza pamoja na kituo cha kupoza Umeme MVA 60 kilichopo Kidahwe wilayani Kigoma mkoani hapa.

AM/MTV News DRC