TANZANIA

MAGARI YAFANYE KAZI YA KUBORESHA ELIMU - MCHENGERWA

FEBRUARI 04, 2024
Border
news image

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania TAMISEMI Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia matumizi ya magari mapya 13 yaliyotolewa na Serikali kuwa yanaleta tija ya kuwahudumia watumishi na wananchi.

Mheshiwa Mchengerwa aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha kushughulikia changamoto za upandishaji wa vyeo na kubadilisha kada kwa walimu katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Mheshimiwa Mchengerwa pia amewataka viongozi hao kote nchini kuhakikisha katika taarifa zao za utendaji kazi wa kila mwezi anapata taarifa ya utendaji kazi wa Maafisa Elimu na Idara ya Afya ili kuona kama magari yaliyotolewa kwa shughuli za ufuatiliaji na utatuzi wa kero za wananchi zinafanyiwa kazi kwa wakati pamoja na Maafisa Elimu kwenda vijijini kutatua kero za walimu.

“Maafisa Elimu fanyeni mikutano na walimu, nendeni mshuke vijijini mkatatue kero na changamotoa za walimu mara moja na zile zilizo nje ya uwezo wenu kazileteni kwetu” Alisema Mheshimiwa Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa alifanya zoezi la kugawa magari 13 yenye thamani ya Zaidi ya Shilingi Bilioni 1.8 yatakayosaidia ufuatiliaji wa masuala ya elimu msingi katika Halmashauri 13 kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (GPE LANES II) na kuwaelekeza viongozi wa Mikoa na Wilaya kufuatilia matumizi sahihi ya magari hayo.

Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa alisema Serikali ilisaini Mradi mpya na Wadau wa GPE ambao una afua za kutatua changamoto za walimu nchini unaojulikana kama ‘Teacher Support Programme’ (TSP) wenye thamani ya shilingi Bilioni 264 ambao umeanza katika mwaka wa 2023/2024 ikiwa ni matunda ya Mheshiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaimarisha mahusiano ya kimataifa na nchi na Wadau mbalimbali wa maendeleo.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo alisema magari yaliyotolewa na Programu ya Kuimarisha Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (GPE LANES II) yatasaidia kuhamasisha utendaji kazi na utekelezaji wa kitaaluma hasa maeneo ya pembezoni kwani yatasaidia kuongeza kiwango cha ufaulo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshiwa Rosemary S. Senyamule akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya mgeni rasmi ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya Serikali na amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuwapatia changamoto ya kwenda kufuatilia miradi ya maendeleo na kero za walimu kwani maelekezo hayo yamezaa matunda kwa kuwa ufanisi unaonekana kwa kukamilika miradi ya maendeleo na kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi na sasa kama mkoa wameandaa Mpango Mkakati wa Elimu wa mkoa na ataukabidhi kweke rasmi.

Naye Peter Fusi Afisa Elimu (Msingi) Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia gari kupitia Programu ya GPE kwani yeye ndiye sauti yao kwa Wadau wa Maendeleo na sasa wataweza kufika maeneo korofi kama yale yanayozunguka Mto Ruaha na Bwawa la Mtera.

MTV Tanzania