TANZANIA

MAANDAMANO YALIYOITISHWA NA CHADEMA YAMEENDELEA KUTIKISA MAENEO MBALIMBALI YA JIJI LA DAR ES SALAAM

JANUARI 24, 2024
Border
news image

Maandamano yaliyoitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yameendelea kutikisa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam huku viongozi, wafuasi na wanachama wakishiriki.

Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kufanyika kwa maandamano hayo leo Januari 24, 2024 akisema lengo ni kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni.

Miswada hiyo ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa yote ya mwaka 2023 na kuishinikiza Serikali kusikiliza maoni ya wananchi na kutaka itengeneze mpango wa dharura wa kukabiliana kwa kupanda gharama za maisha kwa Watanzania.

Maandamano hayo ya amani yameanzia Stendi ya Daladala ya Mbezi Luis yanaelekea ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) hapa nchini huku Jeshi la Polisi likiwa limeimarisha ulinzi njiani kuelekea Barabara ya Morogoro, Shekilango, Igesa - Sinza na kuishia Barabara ya Sam Nujoma ofisi za UN jijini Dar es Salaam.

Tryphon Odace - MTV Tanzania