Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Ndugu Abdulrahman Kinana, ameziagiza kamati za siasa za CCM, kuwafuatilia na kuwachukulia hatua wanachama walioanza kupitapita kusaka ubunge na udiwani.
Amesema wanaofanya hivyo wanakiuka kanuni, utaratibu na miongozo ya uchaguzi ndani ya CCM.
Amesema kwamba watakaobainika hawatapitishwa na vikao vya maamuzi kugombea nafasi hizo, hata kama wataongoza katika kura za maoni.
Kinana ameyasema hayo wilayani Hai, Kilimanjaro katika mkutano mkuu wa jimbo la Hai, uliohusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, jimboni humo.
“Nataka nitumie fursa hii kuziagiza kamati za siasa za CCM nchi nzima, zikisaidiwa na kamati za maadili nchi nzima, kuwafuatilia wale ambao wameanza kuzungukazunguka kutafuta ubunge, udiwani, uenyekiti wa mtaa au kitongoji kuanzia sasa,” ameagiza Makamu Mwenyekiti na kuongeza:
“Hatuna nafasi ya kuhangaishwa na watu wanaotafuta uongozi kipindi hiki, wasubiri hadi mwezi wa saba mwaka 2025, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) itaamua tarehe ya kwenda kuchukua fomu, kabla ya hapo unavunja kanuni".
Amesema mwana CCM asifikiri kwamba akianza kampeni kabla ya wakati, akapigiwa kura akawa wa kwanza, atapitishwa kugombea, hapana, hatapita.
"...alianza kampeni mapema, alitoa rushwa, alikivuruga Chama, hata upate kura za wajumbe wote hutapita," ameonya Ndugu Kinana.
Amebainisha kwamba, kuna vigezo vingi vinatazamwa zikiwamo; kura, uzingatiaji wa maadili na kanuni.
"Je, ulitoa rushwa, ulizingatia kanuni, uliwachafua viongozi wenzako walioko madarakani? Kwa hiyo unaweza ukawa wa kwanza lakini ukawa wa mwisho,” ametahadharisha.
Aidha amewataka wanaccm wote kushirikiana na viongozi waliochaguliwa ambao wana wajibu wa kutekeleza ahadi zilizotolewa na Chama kwa Watanzania.