TANZANIA

Dodoma Yapokea Tani 88 za Sukari

FEBRUARI 26, 2024
Border
news image

Mkoa wa Dodoma nchini Tanzania umepokea jumla ya Tani 88 sukari kupitia kwa Mawakala wake Aidan Gulamali na Mohamed Enterprises (MO)hali iliyomfanya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Rosemary Senyamule kufanya ziara ya kushtukiza ili kutoa maelekezo ya Serikali juu ya uuzaji wa sukari kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma.

Akiwa kwenye duka la Gulamali lililopo eneo la Majengo sokoni Jijini Dodoma, Mhe. Senyamule amesema, "Mhe. Rais ameiona sababu ya kutafuta mbadala wa sukari kwa kumruhusu kutoa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi. Sukari hii hailipiwi kodi Wala VAT ili watanzania waipate kwa gharama nafuu. Wapo Mawakala maalumu wanaotumika kupokea na kusambaza sukari."

Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa maelekezo ya bei elekezi ya kuuza sukari na kusisistiza Sheria itachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kukiuka maelekezo hayo ya Serikali.

"Maelekezo ya Serikali ni kwamba sukari hii iuzwe kwa mgawanyo kila mmoja apate. Iunzwe kuanzia shilingi 2800 mpaka 3000 kwa kilo moja. Kuuza zaidi ya bei elekezi ni kinyume cha Sheria na tutawachulia hatua wale wote watakaobainika kuuza kinyume na maelekezo. Tuifanye sukari kuwa huduma nzuri kwa wananchi" amesisitiza RC Senyamule.

Pia amesema kuna Maafisa kila eneo la Mkoa wa Dodoma watakaofanya ufuatiliaji ili kuhakikisha sukari hii inauzwa ndani ya Mkoa wa Dodoma na si vinginevyo. Hii ni kufanikisha sukari hii inawanufaisha Wanadodoma kwani tayari kuna wafanyabiashara 17 wameshakamatwa kwa kukiuka maagizo.

Mawakala Gulamali na Mohamed Enterprises ni miongoni mwa Mawakala watano wanaohusika na upokeaji pamoja na usambazaji wa sukari Mkoa wa Dodoma ambao leo wamepokea Tani 58 na 30 na kufanya jumla ya Tani 88 ambazo zikigawanywa vizuri na kwa usawa zitawezesha wananchi wote wa Dodoma kupata bidhaa hiyo adhim.

MTV Tanzania