Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Masasi kutumia fedha za mapato ya ndani kujenga jengo kwa ajili ya kuweka mashine ya Mionzi (X-Ray) katika kituo cha afya kata ya Chiwale.
Dkt. Samia ametoa maagizo hayo leo wakati anahutubia wakazi wa Masasi katika mkutano wa hadhara, akitolea ufafanuzi hoja ya Mbunge wa Ndanda Cecil Mwambe, aliyelalamikia changamoto ya ukosefu wa jengo hilo licha ya Serikali kupeleka mashine hiyo ya X-Ray.
“Hivi kweli Halmashauri kama kweli mnataka hii mashine ihudumie watu, mnashindwa kupata Mil. 250/300 kujenga jengo ambalo hii mashine itawekwa na kuweza kuhudumia wananchi, yani kila kitu kila senti itoke Serikali kuu, hamko ‘serious’ hamko ‘serious’ kabisa na maendeleo ya watu.”
“Mmejilemaza, tulisema asilimia 40 ya mapato ya ndani ya kila halmashauri yaelekezwe kwenye shughuli za maendeleo sasa maendeleo mnayofanya nyie na wapi na hizo fedha? Amesema Dkt. Samia.
Madiwani fanyeni kazi yenu ya kuzisimamie Halmashauri, na Menejimenti za Halmashauri fanyeni kazi fedha za Maendeleo zikafanye maendeleo ninyi sio watawala ni Watumishi wa watu’ amesisitosa Dkt. Samia
Kufuatia hali hiyo, Dkt.Samia amewataka watendaji wa halmashauri na madiwani kujitathimini na kutafta fedha shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kujenga jengo hilo.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Mtwara iliyoanza Septemba 14, 2023 na kuelekea Mkoani Lindi.