IVORY COAST

Dkt. Ndumbaro Ateta na Wachezaji Stars Kuikabili Morocco AFCON2023

JANUARI 16, 2024
Border
news image

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo maalumu na kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) kilichoweka kambi katika Jiji la San Pedro nchini Ivory Coast kujiandaa na mchezo wa kwanza wa mashindano ya AFCON 2023 dhidi ya Morocco.

Mhe. Ndumbaro amezungumza na wachezaji hao mara baada ya kushuhudia mazoezi na utayari wa kikosi hicho kuelekea mchezo wao na Timu ya Taifa ya Morocco utakaopigwa jijini humo Januari 17, 2024.

Baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa muda wa takribani saa mbili, Waziri Dkt. Damas Ndumbaro amesema ameridhishwa na maandalizi ya kikosi hicho, Ari na morali ya wachezaji na benchi la ufundi ambayo inatoa picha nzuri ya kufanya vizuri katika kundi F la michuano hiyo.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Bw. Wallace Karia, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) ambaye pia ni Mkuu wa msafara wa timu Bw. Suleiman Mahamoud Jabir.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania