TANZANIA

Dkt. Mashinji - Uwepo wa Faru Umechangia Idadi ya Wageni Kuongezeka Hifadhi ya Taifa Serengeti Tanzania

SEPTEMBA 23, 2023
Border
news image

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara nchini Tanzania Dkt. Vincent Mashinji amesema uwepo wa wanyama Faru katika Hifadhi ya Taifa Serengeti umechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii. Ongezeko la wanyama hao ambao ni kivutio kwa watalii wa ndani na nje limechangiwa na juhudi kubwa za ulinzi zinazofanywa na maafisa na askari wa TANAPA waliojitolea kwa jasho na damu kuhakikisha wanyama hawa adimu wanaendelea kuwepo.

Dkt. Mashinji ameyasema hayo ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Faru duniani yaliyofanyika Fort Ikoma wilayani Serengeti kwa kushiriki mbio fupi kwa ajili ya kuadhimisha siku hii. Na kusema, "nimefurahi kuambiwa kuwa wanyama hawa adimu idadi yao inaongezeka mwaka hadi mwaka, ongezeko la wanyama hawa limeendelea kuvuta watalii wengi sana wa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Niwahakikishie kama Mkuu wa wilaya hii ya Serengeti nitashirikiana na TANAPA kukilinda kizazi hiki cha Faru kisitoweke".

Aidha, nawapongeza sana maafisa na askari kwa kuwatunza Faru hawa, kwa kuwa idadi inaendelea kuongezeka niwaombe kushirikiana na jamii inayozunguka hifadhi hii, watoe taarifa pale wanapowaona wakiwa nje ya maeneo ya asili ili wasiuwawe na majangili wasioutakia mema uhifadhi.

Hata hivyo Dkt. Mashinji aliwashauri TANAPA kuona kama kuna uwezekano wa wanyama hao pia, kuongezwa na kuhifadhiwa katika Hifadhi za Taifa Burigi-Chato, Arusha na Nyerere ili watalii wenye shauku ya kuwaona Faru wawe na machaguo mengi zaidi badala ya Serengeti na Mkomazi kama ilivyo sasa.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Albert Mziray akimkaribisha mkuu wa wilaya hiyo, alitoa pongezi kwa wawekezaji kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha kazi hii adhimu ya Uhifadhi na utunzaji wa Faru.

" Nichukue nafasi hii kuwapongeza Frankfurt, WWF, Friends of Serengeti na majirani zetu TAWA kwa kuja kwenye maadhimisho haya. Pia kwa mchango mkubwa mnaoutoa katika kufanikisha utunzaji wa Faru hawa na shughuli zote za Uhifadhi kwa ujumla".

Akifafanua kwa niaba ya Mratibu wa Faru Taifa Mhifadhi Mkuu Emmanuel Kaaya amesisitiza tuendelee kuweka jitihada katika ulinzi wa Faru na ulinzi huu unaendelea kuimarishwa ili kutimiza malengo ya Uhifadhi wa FARU haswa katika kutekeleza mkakati wa FARU Taifa.

Aidha, Kaaya alisema, “tutawapa tuzo washindi wa mbio za asubuhi pamoja na watumishi waliojitolea usiku na mchana kuwahifadhi Faru kwa mwaka huu 2023 tunafanya hivi ili kuenzi na kuheshimu mchango wenu”.

Maadhimisho haya yamefanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa kuanza na mbio zilizohamasisha utunzaji wa Faru na kuongozwa na kauli mbiu inayosema

"Tuwalinde Faru dhidi ya Ujangili ili tuongeze idadi yao."

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania