Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati nchini Tanzania Mhe. Dkt.Doto Biteko amezitaka kampuni za Bima nchini kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuwajengea uwezo Wananchi kufahamu faida ya kuwa na bima zitakazowasaidia katika nyanja mbalimbali ikiwemo makazi na usafiri.
Dkt.Biteko ameyasema hayo wakati akizungumza na Watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati Jijini Dar es Salaam.
"Elimu ya bima kwa wananchi bado haijaeleweka vizuri, hivyo nendeni mkatoe elimu ili wananchi wapate mwamko wa kukata Bima ya rasilimali zao, msijikite kwenye kutafuta masoko tu," amesema Dkt. Biteko.
Amefafanua kuwa ili kuendelea kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla, kampuni za Bima zinatakiwa kutunza fedha zake kwenye Benki za ndani ya nchi jambo ambalo litachochea maendeleo.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Katibu Mkuu Kiongozi Mha. Zena Ahmed Said ambaye pia ni Balozi wa Bima Tanzania amesema Mamlaka inaendelea na mkakati wa kutoa elimu kwa umma kwa kushirikiana na mashirika ya Serikali na Sekta Binafsi.
Amesema kuwa, lengo ni kuwafikia watanzania asilimia 80 wenye zaidi ya umri wa miaka 18 ifikapo mwaka 2030 pia Mamlaka inaendelea na hatua ya kuhamasisha Wizara na Taasisi za Serikali ziweke Bima kwenye miradi inayotekelezwa katika Sekta hizo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba pamoja na Mabalozi wa Bima nchini.