TANZANIA

BMH YATOA MKONO WA EID KWA YATIMA

Aprili 10, 2024
Border
news image

Hospitali ya Benjamini Mkapa nchini Tanzania (BMH) imetoa vyakula kwa Kituo cha yatima cha Rahman cha Chang'ombe jijini Dodoma kama mkono wa Sikukuu ya Eid-el-Fitr.

Vyakula hivyo vimejumuisha mbuzi wawili, kilo 50 za mchele, kilo 50 za unga wa ngano pamoja na juisi katoni 10 na maji katoni 20 vimekabidhiwa kwa kituo hicho na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Dkt Alphonce Chandika.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vyakula hivyo, Dkt Chandika, amesema BMH pamoja na kutoa huduma za afya, lakini wana wajibu wa kurudisha kwa jamii na kulea jamii inayowazunguka.

"Tumeona tuwakabidhi watoto yatima vyakula kama mkono wa Eid-el-Fitr ili nao waweze kusherehekea sikukuu kama watoto wengine," amesema Mkurugenzi Mtendaji, wakati akiongea na waandishi wa habari baada ya kukabidhi vyakula hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, aliambatana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Hospitali, Prisca Lwangili, na Mwanasheria wa Hospitali, Advocate Alfred Kanan.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo, Rukia Hamis, anasema Kituo kilianza mwaka 1998 kwa ajili ya kutatua changamoto za kinamama.

"Mwaka 2006, tukaona pia tutoe malezi kwa watoto wanaopitia changamoto hivyo tukaanza na watoto 15, Sasa hivi tuna watoto 150," anasema.

Bi Rukia ameishukuru BMH kwa msaada huo na kuziomba taasisi nyingine ziige mfano wa BMH kwa kuwakumbuka watoto yatima nyakati za sikukuu ili watoto hao nao waweze kufurahi kama wengine.

MTV Tanzania