TANZANIA

SERIKALI YA TANZANIA KUANDAA BEI LINGANISHI YA MAFUTA

JANUARI 31, 2024
Border
news image

Serikali ya Tsnzania ipo katika maandalizi ya kupanga bei linganishi ya Mafuta ya Dizeli, Petroli na Taa nchini, jambo litakalosaidia wananchi waishio mikoa ya pembezoni kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alipokuwa jijini Dodoma, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo kuhusu majukumu, mafanikio na changamoto za EWURA.

"Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea na mikakati ya kupanga bei linganifu ya Mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa kwa ajili ya kuondoa utofauti uliopo kati ya mkoa mmoja hadi mwingine wakati wa ununuzi wa Mafuta," amesema Kapinga.

Ameeleza kuwa Serikali imeanza kuwekeza kwenye mifumo ya kieletroniki ikiwemo Ujenzi wa miundombinu mipya ya kisasa katika maeneo tofauti tofauti nchini ili kuweza kufanikiwa kupanga bei linganifu ya Mafuta.

Kapinga amefafanua kuwa taratibu za kupanga bei linganishi ya Mafuta katika bandari ya Dar es salaam, Mtwara na Tanga zimekamilika na zitaanza kutumika mwezi Machi mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo, Mhe. Dkt. Jasson Samson Rweikiza ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo ya kuanza utaratibu wa kupanga bei linganishi ya Mafuta ya Dizeli, Petroli na Taa kwa nchi nzima na kusisitiza kuwa jambo hili litaleta nafuu kwa wananchi waishio katika mikoa ya pembezoni mwa nchi kama Kagera, Kigoma na Mtwara.

Semina hiyo imehudhuriwa na Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Oliver Nyeriga-MTV Tanzania