Askari wahifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) nchini Tanzania siku ya Septemba 11, 2023 walifanikiwa kumuokoa mtoto wa tembo anayekadiriwa kuwa na umri wa wiki nne (4) aliyezama katika shimo lenye matope katika Kijiji cha Kwamsanja kilichopo kata ya kibindu halmashauri ya Chalinze jirani na Pori la Akiba Wamimbiki.
Taarifa za Mtoto huyo wa tembo aliyetelekezwa na kundi lake kutumbukia shimoni zilitolewa na raia mwema aitwaye Manase Thomas Baha mkazi wa Kijiji cha Kwamsanja na kumlazimu Kamanda wa Pori la Akiba Wamimbiki Emmanuel Lalashe kutuma timu ya askari wanne (4) walioshirikiana na askari wa Jeshi la Akiba (migambo) sita (6) kwa ajili ya zoezi zima la kumuokoa mtoto huyo wa tembo.
Akizungumza baada ya zoezi la uokoaji, Kamanda Emmanuel Lalashe aliwashukuru wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi ya Wamimbiki kwa ushirikiano wanaoutoa katika kulinda rasilimali za Nchi yetu zilizopo katika hifadhi hiyo hususan rasilimali Wanyamapori ambazo ni chachu ya shughuli za Utalii na Pato la Nchi.
Mahusiano mazuri yaliyojengwa kati ya wahifadhi wa hifadhi ya Wamimbiki na wananchi wanaoishi vijiji Jirani na hifadhi hiyo umekuwa na manufaa makubwa siku za hivi karibuni kwani wananchi wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa katika shughuli za uhifadhi.