TANZANIA

Aphfta Leteni Vigezo Vyenu Tujadiliane Kwenye Kamati

MACHI 01, 2024
Border
news image

Waziri wa Afya nchini Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu ameutaka Uongozi wa APHFTA kuwasilisha vigezo vyao vya kupinga maboresho ya vitita vya mafao kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya yaliyoanza kutekelezwa leo Machi 1, 2024.

Waziri Ummy amesema kuwa Wizara iliamua kusitisha utekelezaji wa Kitita kipya cha NHIF na pia kuunda Kamati ya Wataalam kutoka Serikalini, Sekta binafsi na Taasisi za Bima kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusu hoja za APHFTA na NHIF. Kamati hiyo iliongozwa na Dkt. Baghayo Saqware, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Nchini (TIRA).

Amesema kuwa Kamati iliundwa kwa lengo la kufanya mapitio ya bei na kuandaa vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya Kitita hicho bila kuathiri upande wowote. Kamati ilibainisha vigezo mbalimbali katika kukotoa gharama za huduma. Kwa Huduma za Dawa, Kamati ilibainisha vigezo vikuu vitatu;-

a. Bei ya jumla ya soko ya dawa nchini b. Gharama za uendeshaji na

c. Kiwango cha faida

Na kwa upande wa Vipimo na huduma za upasuaji, Kamati imebainisha vigezo 6 vifuatavyo:-

a. Bei ya soko katika ununuzi wa vifaa na vitendanishi

b. Idadi ya vifaa na vitendanishi vinavyohitajika

c. Rasilimaliwatu inayohitajika na muda unaotumika kutoa huduma

husika

d. Kiwango cha uchakavu wa vifaa vinavyotumika

e. Gharama za uendeshaji

f. Kiwango cha wastani wa faida.

Waziri Ummy ameitaka APHFTA kurudi nyuma na kukaa mezani na Kamati ili kupitia vigezo wanavyopendekeza.

MTV Tanzania