Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati nchini Tanzania Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki kuhusu miradi mbalimbali ya umeme inayofadhiliwa na benki hiyo pamoja na miradi mingine ya nishati iliyo katika mpango wa kufadhiliwa.
Mazungumzo hayo ambayo yamefanyika Jijini Dodoma pia yamehudhuriwa na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba.
“Benki ya Maendeleo Afrika imeonesha nia ya kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo ya usafirishaji na usambazaji umeme na kubwa zaidi katika hili, wameamua kuweka kipengele cha nishati safi ya kupikia kwenye mipango yao, na hii ni katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema AfDB imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo mradi wa umeme wa Kakono wa megawati 87.8 kwa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 161 na mradi wa Malagarasi wa megawati 49.5 kwa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 120.
Amefafanua kuwa, Benki hiyo pia imetoa sehemu ya fedha za utekelezaji wa miradi ya usafirishaji umeme ukiwemo mradi wa Singida-Arusha-Namanga (kV 400) ambao sasa umefikia asilimia 99, mradi wa Rusumo-Nyakanazi (94 km) ambao umekamilika kwa asilimia 100 na mradi wa umeme wa Backbone unaojumuisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme mkoani Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo kituo cha Dodoma na Singida vimekamilika kwa asilimia 100.
Kufuatia hatua hiyo, Dkt.Biteko ameishukuru AfDB kwa kutoa sehemu ya fedha ambazo zinatekeleza mradi wa usafirishaji umeme wa kV 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma ambao sasa umefikia asilimia 92.
AfDB pia imeonesha nia ya kufadhili mradi wa usambazaji wa Gesi Asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam kwa kutumia mfumo wa ushirikiano na Sekta Binafsi (PPP).
Pia AfDB imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali katika mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ya kV 220 sambamba na kushirikiana na serikali katika uendelezaji miradi mbalimbali ya nishati jadidifu.
Dkt. Biteko amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni fursa adhimu itakayowezesha Taifa kuwa na nishati ya kutosha kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki, amesema nia ya Benki hiyo ni kuhakikisha miradi ya umeme inayofadhiliwa na AfDB inakamilika kwa wakati ili kuwapa wananchi umeme wa uhakika.
Ameongeza kuwa, Benki hiyo itaendelea kufanya tathmini kuona namna ya kuendeleza mipango mbalimbali ya Tanzania kwenye gesi asilia ikiwemo kupitia mpango mkakati wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili kuainisha maeneo zaidi ya ushirikiano.