Tanzania

Acheni Kuwatoza Wagonjwa Posho Za Dereva Kwenye 'Ambulance'

JULAI 29, 2024
Border
news image

Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu amekemea vikali na kuwaonya viongozi wa Hospitali zote nchini zenye magari ya kubeba wagonjwa (Ambulance) waache tabia ya kuwatoza wagonjwa au ndugu zao malipo ya posho ya Dereva na mtaalam anaesindikiza mgonjwa kwenye rufani.

Waziri Ummy amesema hayo Julai 28, 2024 jijini Tanga wakati akikabidhi gari la kubeba wagonjwa (Ambulance) kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga - Bombo ambalo ni sehemu ya magari 736 yaliyonunuliwa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Ni marufuku kwa Hospitali zote nchini kuwatoza wananchi pesa ya posho ya Dereva wala Muuguzi anayemsindikiza Mgonjwa na badala yake Mwananchi anapaswa kuchangia gharama za mafuta tu na sio vinginevyo." Amesisitiza Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesisitiza matumizi sahihi ya magari hayo ambapo amekataza yasitumike kinyume na shughuli za wagonjwa pale inapohitajika ili yaendelee kudumu na kutoa huduma kwa Watanzania kwa kuimarisha huduma za rufani na dharura kwa ngazi zote.

"Magari haya yamenunuliwa kwa gharama kubwa sana, yatunzwe kwa kutenga fedha za matengenezo ya kawaida (Service) pamoja na kuyakatia Bima kwakuwa yamekuwa yakipata ajali mara kwa mara." Amesema Waziri Ummy

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Imani Clemency amesema, kufuatia uwepo wa huduma hii kwa kila Halmashauri, wamejipanga kuimarisha huduma za rufaa hususani kwa akina mama wajawazito ambapo wameanzisha huduma ya simu ya dharura ya bila malipo namba 115, mwananchi atapiga na kupatiwa huduma haraka.

AM/MTV News DRC