TANZANIA

WADAU WATOA MISAADA YA KIBINADAMU RUFIJI TANZANIA

Aprili 10, 2024
Border
news image

Mbunge wa Rufiji na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania Mhe. Mohamed Mchengerwa ameshiriki utoaji wa misaada ya chakula na malazi kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea katika Wilaya ya Rufiji.

Mhe. Mchengerwa akiwa na Uongozi wa CCM Mkoa wa Pwani pamoja na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dkt. Mehmet Gulluoglu wametoa misaada hiyo kwa wakazi wa Mohoro walioathirika na mafuriko ambao wamejihifadhiwa katika Shule ya msingi Mohoro.

Akizungumza na wananchi Mchengerwa amesema "Tunatambua athari zilizoletwa na mafuriko haya kaya nyingi zimeathirika nilikwishatoa Sh.Milioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa mbegu kwa wananchi walioathiriwa mashamba yao na mvua lakini kama hiyo haitoshi rafiki zangu wameniunga mkono na sasa tumeleta vyakula pamoja na magodoro kwa kaya zinazoishi katika shule hii."

Ameongeza kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anafahamu taarifa hizo na ametuma Timu ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kufika eneo hilo na kukuendelea kutoa misaada ya kibinadamu katika kata 12 za Wilaya ya Rufiji na kufanya tathmini ya kina ya athari ya mafuriko hayo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao ametoa rai kwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kuhakikisha anasimamia vyema misaada hiyo kwa kuweka mpango wa kuhakikisha wale wenye uhitaji zaidi ndio wanaopata na sio wale wenye kuhitaji nyongeza.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dkt. Mehmet Gulluoglu amesema wameguswa na adha hiyo iliyowapata wananchi wa Rufiji na ametoa msaada wa vyakula na bahasha ya pole kwa familia zilizothirika zaidi.

MTV Tanzania