TANZANIA

UJENZI WA BARABARA YA SANZATE - NATA WAFIKIA 45%

Aprili 06, 2024
Border
news image

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi imesema inaendelea na ujenzi wa barabara ya Sanzate - Nata iliyopo Wilaya ya Serengeti mkoani Mara (km 40) kwa kiwango cha lami ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 45 na inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Januari, 2025.

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Serengeti Jeremiah Amsabi aliyehoji Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya lami kipande cha Sanzate hadi Natta.

"Mheshimiwa Spika baada ya Waziri kutembelea na kuongea na Mkandarasi, kimefanyika kikao na watendaji wake wakuu na kumekuwa na mabadiliko na tayari Mkandarasi yupo site anaendelea na kazi, na kuhusu malipo nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari maandalizi ya malipo ya certificate za mkandarasi yapo na ndio maana yupo 'site', amesema Eng. Kasekenya.

Eng. Kasekenya amesema mpango wa Serikali ni kuijenga barabara yote kutoka Mugumu - Natta - Sanzate hadi Makutano kwa kiwango cha lami ili kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wa Serengeti na maeneo jirani.

Aidha, Eng. Kasekenya amesema Barabara ya Kilindoni - Rasi Mkumbi wilaya ya Mafia mkoani Pwani ipo kwenye mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na itajengwa kwa kiwango cha lami.

Eng. Kasekenya ameeleza hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Hawa Mchafu aliyeuliza ni lini Serikali itajenga Barabara ya Kilindoni - Rasi Mkumbi itajengwa kwa kiwango cha lami.

MTV Tanzania